LIVING WATER CENTRE MINISTRY

hghost

ROHO MTAKATIFU

Kama kanisa limeitwa kuakisi/kurejesha Utukufu wa Mungu, basi linamwitaji mwenye huo utukufu aweze  kutimiliza hilo. Chanzo cha huo utukufu ni Roho Mtakatifu. Yeye ndiye mbebaji na anapokaa ndani ya mwamini ndipo huwa na fursa ya kutekeleza hilo. I Korintho 3:18 (angalia somo la KUAKISI UTUKUFU WA BWANA).

Huyu Roho Mtakatifu ni nani? Umuhimu wake ni upi? Kazi zake ni zipi?

 1. Roho Mtakatifu ni Muumbaji

Mwanzo 1:2

Ayubu 33:4

Kama  siyo Yeye, chochote ukionacho/usichokiona kisingekuwepo. Ulimwengu uliumbwa na Yeye na wewe uliumbwa na Yeye. Anaujua ulimwengu na anakujua kuliko yeyote yule. Anapaswa kuwa ‘partner’ wa maisha yako kuliko mwingine yeyote maana bila Yeye huna ‘future.’

Roho Mtakatifu haingilii chochote kinachokuhusu au kukuzunguka kwenye maisha yako kabla hajamaliza kukushughulikia wewe binafsi. Anakufinyanga na kukufanya uwe bora ndipo aanze kuyangilia yanayokuhusu kama uchumi, mahusiano, kazi, huduma, elimu n.k.

II Petro 1:21 Wanadamu watakatifu wakiongozwa na Roho Mtakatifu

Yohana 14:26 Kusingekuwepo na Agano Jipya bila Roho Mtakatifu

Yohana 15:26-27 Alikuwepo tokea mwanzo

 1. Roho Mtakatifu ni Nafsi kamili

Kama vile alivyo Mungu Baba na Mungu Mwana ndivyo alivyo Mungu Roho Mtakatifu. Ni nafsi inayojitegemea katika utatu mtakatifu. Anayo maamuzi yake na utaratibu wake wa utendaji kazi. Roho Mtakatifu ana tabia, utashi na hisia. Ni nafsi kamili!

Yesu alipokuwa na wanafunzi wake, hawakuwa na nguvu hadi Roho Mtakatifu alipokuja. Anavyo vitu ambavyo Yeye asipokuwapo hakuna vitakavyoonekana. Ni Roho kamili.  Matendo 1:8 Nanyi mtapokea nguvu akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu nanyi mtakuwa mashaidi wangu Yerusalemu, Uyahudi, Samaria na mpaka mwisho wa nchi.

Ebrania 9:14       Roho anawezesha kazi ya msalaba

I Petro 1:2           Utakaso hufanywa na Roho pia

Warumi 8:27       Roho anawaza, anatafakari na hufanya maombi

Warumi 15:30     Roho anao upendo, anaweza kupenda na kufurahia  ushirika na mwamini

II Kor 12:11        Anao utashi (will), anayo maamuzi ya kufanya vitu kama apendayo/achaguavyo Yeye.

 1. Roho Mtakatifu ni Wakala wa Wokovu (Agent of salvation)

Uwakala ni kusimamia mahali pa kuunganisha watu/jamii na huduma fulani

Moja ya kazi za Roho Mtakatifu ni kuhakikisha watu wanaokoka. Anaelezea na kufafanua uzuri wa wokovu ulivyo na kumwezesha mhusika kuweza kuupokea. Hufanya hivi kwa namna zifuatazo:-

 1. Huhukumu ulimwengu na dhambi

Yohana 16:7-8

Ile hali ya kujisikia ni mkosaji una dhambi na kuhitaji toba, huletwa na Roho Mtakatifu. Anaachilia kioo cha kujiona una dhambi ili utubu. Hata baada ya kuokoka mtu akifanya dhambi, lazima Roho Mtakatifu atamshuhudia kuhusu  hilo kosa ili alitubie. Huwasha ‘red light’ pale unapotaka kufanya dhambi ili uepukane nayo. Roho Mtakatifu ni wa Agano la milele, akiingia huendelea kutusaidia.

 1. Hutufunulia Kweli juu ya Kristo Yesu

Yohana 14:16, 26

Ili Yesu aweze kukubalika, kutambulika na kuhitajika, lazima Roho Mtakatifu alifanye hilo kwa mhusika. Hili ni muhimu kwa maisha yako binafsi na pale unapowafikishia wengine Injili. Neno hili Kufunua lina maana ya kuweka wazi, kurahisisha na kuelewesha (hasa maneno ya Yesu).

 1. Hutupa kuzaliwa mara ya pili (kuzaliwa upya)

Yohana 3:3-6

Anayeizaa roho ya mhusika mara ya pili ni Roho Mtakatifu. Yeye ni Roho hivyo huweza kuishughulikia roho ya mwanadamu ipasavyo. Roho Mtakatifu hufanya kazi pamoja na Neno lililoingia ili kumzalisha mtu mara ya pili.

 1. Roho Mtakatifu ni Wakala wa Utakaso (Agent of sanctification)

Hakuna utakatifu bila Roho Mtakatifu!

Warumi 8:2-4

Yale yasiyowezekana kwa sheria, Roho ameyakweka sawa. Yeye ndiye atutengaye na sheria ya dhambi na mauti na kutuweka huru.

II Thesalonike 2:13 Roho ndiye asababishaye utakaso utokee.

Huyu ndiye Roho atupaye kushinda dhambi. Pasipo Yeye dhambi itakutesa maisha yako yote.

 1. Anatuita na kutukumbusha kwamba tu watoto wa Mungu

Warumi 8:16

Roho Mtakatifu huzijulisha na kuzishuhudia roho zetu ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu. Asipofanya hivyo, utakosa uhakika na ujasiri ya kujua kuwa wewe ni mtoto wa Mungu. Ni muhimu kwa mwamini popote alipo ajijue kuwa Baba yake ni Mungu na amezaliwa naye.

 1. Hutusaidia katika Ibada yetu kwa Mungu

Matendo 10:46

Roho Mtakatifu ndiye awezeshaye mwamini kumwabudu Mungu.

Huziongoza na kuzinidhamisha roho zetu kufanya ibada

atakayo Mungu. Pasipo Yeye ibada hubaki kuwa ya kimwili na

kwajinsi hiyo haiwezi kumgusa Mungu.

 1. Hutusaidia katika Maombi na Kutuombea

Warumi 8:26-27

Kazi hii huifanya kwa ushirika na roho ya mwamini, na huifanya kutokea ndani. Ni muhimu kwa mwamini kuruhusu kutawaliwa na Roho Mtakatifu pale afanyapo maombi. Hii itasaidia maombi yake yawe na majibu ya uhakika kwa kuwa Roho hujua kile atakacho Mungu.

 1. Kuzalisha sura ya Kristo ndani ya mwamini na zile tabia zimtukuzazo Kristo

Wagalatia 5:22-23

Tunda la Roho linaonyesha tabia za kufanana na Kristo. Ushirika na Roho Mtakatifu kupitia Neno huzizalisha tabia hizi na kuleta mafanikio ndani yetu na kwa mahusiano yetu na wengine.

 1. Kutufundisha na kutuongoza katika Kweli yote (Ualimu wa Kiungu)

Yohana 16:13

Roho Mtakatifu huleta ufafanuzi, uelewa na ufahamu wa Kweli ya Mungu. Pasipo Yeye huwezi kuijua Kweli na kuishi sawasawa nayo. Akiisha ingia ndani, tamaa/hamu ya dhambi huanza kuondoka na kwa kupitia Neno lililoko ndani ya mwamini huweza kumfanya awe kama alivyokusudiwa. Pasipo Neno kuwepo ndani, Roho Mtakatifu hana cha kufanyia kazi.

 1. Hupanda Penzi la Mungu ndani ya mwamini

Rumi 5:5

Penzi la Mungu ni muhimu kwa mwamini ndani yake, na Roho Mtakatifu ndiye hulianzisha. Hili ni penzi lisilo na sababu. Hutufanya tupende kama apendavyo Mungu, kwa kuwa tunajua jinsi Mungu atupendavyo.

 

CategoryMASOMO YA VIJANA
© 2016 Living Water Centre | Designed by Consuming Fire Technologies.
Top
Follow us: