PROFESSIONALS (WANATAALUMA)

Mtume Onesmo Ndegi aligundua mambo matatu (3) kuhusu wanataaluma ambao wameokoka, nayo ni:-

  1. Wanataaluma hawapewi nafasi kanisani kutumia taaluma zao
  2. Wanataaluma hawazitafuti hizo nafasi
  3. Wanataaluma hawajui kuziunganisha taaluma zao na ujenzi wa Ufalme wa Mungu.

Hii ndiyo mojawapo ya sababu ya kuamua kuanzisha shirikisho la wanataaluma lenye lengo la kusimama kwenye zamu zao kama wanataaluma wanaomjua Kristo na wanaozitumia taaluma zao kwenye Ufalme Wake.

Mungu alikuokoa ili ufanye partnership (ushirika) na Yeye kupitia mtumishi wake na kazi yake. Yeyote aliyepewa vingi atadaiwa vingi. Ni muhimu kutokuwa mtu wa kukosoa ubovu wa kanisa bali tengeneza eneo unaloweza kwa taaluma yako.

Mtume Ndegi ameitwa na Mungu kwa kazi ya Ufalme, anakuhitaji wewe pia uungane naye siyo tu kwa matoleo (sadaka)yako bali pia taaluma yako. Ipo mifano mingi ya kwenye Biblia ya watu wa Mungu waliotumia taaluma zao na upako wa Roho Mtakatifu katika ujenzi wa Ufalme.

Kutoka 35:30-35   Bezaleli alikuwa na Roho wa Mungu katika hekima, akili, ujuzi na kazi za ustadi kila aina. Kufanya kazi za dhahabu, za fedha na shaba.

Kutoka 18:1-27 Yethro (baba mkwe wa Musa) alimpa Musa mtumishi wa Mungu Ushauri wa kitaalamu wa masuala ya utawala.

Mtume Ndegi amekuwa akiandaa semina maalum za Wanataaluma ili kuwasaidia wasiwe wakristo wa kawaida tu bali wenye kuangalia fursa na mapengo kanisani na kuyaziba kwa taaluma zao. Semina hizi zimekuwa zikifanyika ndani na nje ya Living Water Centre – Makuti Kawe. Mchungaji anahitaji ushauri wa kikandarasi hasa anapojenga kanisa na mtu wa kwanza kumsaidia ni mkristo mkandarasi wa mahali pale. Yapo maeneo mengi kanisa linahitaji taaluma za wakristo wake ili liwe bora zaidi kama masuala ya kisheria, kihasibu, kiualimu, kidaktari, kiulinzi, kisayansi, kijamii n.k

Kanisa la Living Water Centre kwa sasa linao ushirika wa wanataaluma ambao wameamua kutendea kazi suala hili. Ushirika huu umeanza kwa kuwa na vikundi vidogovidogo vya kujifunza na kujadili Biblia (bible group discussions for professionals) vyenye lengo la kuwakutanisha wanataaluma pamoja kwa kuzijenga roho zao ili waweze pia kumtumikia Bwana kwa taaluma walizo nazo.