LIVING WATER CENTRE MINISTRY

praisejesus

KUAKISI UTUKUFU WA BWANA

I Korintho 3:18

Kikawaida unaposimama mbele ya kioo na kujiangalia, utaiona sura na umbo lako kwa namna ile ile ulivyo. Hii huitwa taswira au ‘image’ ambayo hutokea baada ya kuakisiwa (kurudishwa) kwa mwanga kutoka kwenye kioo. Mwanga huu ulitoka kwako au chombo (object) kilichosimama mbele ya kioo. Kisayansi huitwa Kuakisi.

 

Mwamini anapaswa awe wa jinsi hii, yaani aakisi/aurudishe Utukufu wa Bwana kama vile kwenye kioo. Biblia inasema tunabadilishwa tufanane na huo utukufu wa Bwana. Hatubaki na utukufu mmoja, bali tunatoka utukufu hadi utukufu. Utukufu huo chanzo chake ni ROHO MTAKATIFU, aliye BWANA. Kwa hiyo tunamwitaji Roho ili kuliishi hili.

Kubadilishwa huku ili tufanane Naye hutokana na kuyaishi maisha ya Neno, Maombi na Ushirika wetu na Roho.

Mathayo 17:2

Yesu alibadilika kiutukufu ndani nje. Alikuwa anaakisi/anarudisha ile sura/taswira ya BABA akaaye ndani yake. Aliruhusu alichobeba ndani kionekane kwa nje hadharani na kwa uhalisia. Marko 9:3 inaelezea kwa namna ya kwamba kilichokuwa ndani kilidhihirika katika mwili wake, na mwili ulipogusa nguo nazo zikabadilishwa. Kama nguo iliyogusana naye ilibadilishwa, basi chochote kigusanacho nami kinapaswa kupata huo utukufu. Unachokibeba ndani ndicho unachoweza kudhihirisha nje kama utukufu.

Zaburi 19:1

 

Utukufu wa Mungu = Uhalisia/Nguvu/Mamlaka/Utawala wa Mungu alivyo

Utukufu ni yale mambo ukiyaona yanadhihirisha jinsi Mungu alivyo mkuu. Ni yale mambo yanayoelezea Mungu ni wa namna gani.

Kolosai 1:15-16

Kwa lugha ya kiingereza ni kusema “Jesus is the Image of the Invisible God” yaani Yeye anamdhihirisha Mungu asiyeonekana. Ukimwona Yesu umemwona Mungu. Kwa maana hiyo, mwamini anapaswa kumdhihirisha Yesu ili watu wakikuona wewe wawe wamemwona Kristo. Katika Efeso 1:22-23 inaonyesha kuwa Mungu Baba aliweka vitu vyote chini ya Mungu Mwana kwa ajili ya Kanisa ambalo ndio mwili wake na ukamilifu wake. Kama vile Baba alimwitaji Mwana ili amdhihirishe, ndivyo Mwana anamwitaji mwamini ili amdhihirishe. Yesu anasema Kanisa ndio mwili na ukamilifu wake. Hivyo pasipo wewe mwamini Yesu hana mwili na pasipo wewe mwamini Yesu hajakamilika. Huku kunaitwa kuhitajiana na kukamilishana. Hapa ndipo utajua umuhimu wa wewe kukaa kwenye nafasi yako ili uweze kuakisi Utukufu wa Bwana, wengine wapate kumjua Yeye kupitia wewe.

Yesu ni mzaliwa wa kwanza (ni kichwa) na sisi  ni mwili uliofuata alipozaliwa. Kichwa kilipo ndipo wewe mwamini ulipo. Isaya 9:6 inasema kwa ajili yetu Mtoto amezaliwa, tumepewa Mtoto mwanamume na uweza wa kifalme utakuwa Mabegani (kwenye mwili) mwake. Hii ina maana uweza na mamlaka ya kifalme ameliachia kanisa lake! Kwa hiyo unaweza kusema Mungu ana Mtoto mmoja tu aitwaye Kristo (Yesu + Kanisa).

Ebrania 1:3-4      Yesu ni udhihirisho wa utukufu wa Mungu

Eseso 2:6            Nimeketi pamoja Naye katika mkono wa kuume wa Ukuu

Efeso 1:4            Kilichomfanya Yesu awe bora kupita malaika ni kuwa na Jina bora kuliko lao. Na wewe ni bora kuliko malaika kwa sababu unalo Jina kuu ndani yako, nawe unalimiliki na ni lako.

Yesu hakufanya lolote kwa ajili yake bali kwa ajili yako. Kuakisi utukufu

wa Yesu ni kudhihirisha kile Yesu alichofanya kwa ajili yako. Mungu

anataka kujionyesha hadharani kupitia wewe na wengine wanufaike na

uwepo wa wana wake. Utukufu huu hutokana na Roho, maana pasipo Yeye

usitazamie chochote. Lazima umtengenezee makao aje, akae na atawale. Kila

mmoja wetu lazima ajengwe katika ushirika na Roho Mtakatifu, na uwe wa

kudumu. Kujaa Roho hadi kupoteza utawala wa maisha yako, Yeye atawale.

Tena utaratibu wa Roho ni kwamba, huanza kukubadilisha kwanza ndani

yako na akiisha kumaliza hubadilisha kila kitu kinachohusu wewe yaani

uchumi, mahusiano, afya, kazi,hudumu n.k.

Mtume Onesmo Ndegi

06 Januari 2014

Ibada ya Jumapili

 

CategoryMASOMO YA VIJANA
© 2016 Living Water Centre | Designed by Consuming Fire Technologies.
Top
Follow us: