WASIFU WA MTUME ONESMO NDEGI

apostleMtume Onesmo Nyakura Ndegi ana mke mmoja Mchungaji Lilian Ndegi, na wamebarikiwa kuwa na watoto saba; Daniel, Salome, Brian, Brighton, Brigitte, Bora na Blessing. Yeye ndiye Mwanzilishi na Mbeba Maono mkuu wa kanisa la Living Water Centre duniani. Makao makuu ya huduma hii yapo Kawe, Dar es Salaam katika kanisa linalofahamika kama “Makuti Kawe.”

Mtume Ndegi aliokoka na kumjua Mungu wakati akiwa mwanafunzi wa chuo cha Uhasibu, Mbeya (TIA). Kabla ya kuingia rasmi katika huduma, aliwahi kuwa mfanyakazi wa serikali na ofisi yake ya mwisho alikuwa afisa ugavi (procurement officer) katika Wizara ya Mambo ya Ndani. Baadaye aliamua kuacha kazi ya kuajiriwa na kuwa mfanyabiashara mkubwa, akimiliki biashara kadhaa jijini Dar es Saalam. Kipindi chote hiki alikuwa mwaminifu kwa mchungaji wake, na alitumia mali zake kuujenga ufalme wa Mungu ikiwemo kujenga makanisa, kuwezesha mikutano ya injili na kuwategemeza watumishi wa Mungu.

Mungu alipomwita katika huduma haikuwa rahisi kukubaliana na Wito na Kusudi hilo, kwani alipitia kipindi kigumu sana kiuchumi na alipomtafuta Mungu alipewa sababu ya ukame huo ya kuwa ni matokeo ya kukaidi sauti ya Bwana. Huo ulikuwa ni mwaka 1997. Baada ya kuukubali wito huo, Bwana alimrejesha katika hali nzuri ya kiuchumi tena na biashara zake zikastawi, akiwa amepewa maelekezo kuwa muda wa kuanza huduma utakapofika atajulishwa na Bwana mwenyewe.

Mwaka 2000, Bwana alimtaka afunge biashara zake zote na kufungua huduma rasmi. Hivyo, baada ya kufunga biashara zake kwa siku moja aliamua kutumia fedha zake zote alizokuwa nazo bank kununua kiwanja kwa ajili ya kanisa, vifaa vya muziki na mahitaji mengine ya kihuduma. Hii ilisababisha baada ya muda mfupi kurudia tena kwenye kipindi kigumu kiuchumi ambacho kilimwathiri yeye na familia nzima. Watoto wake waliokuwa wakisoma shule nzuri (English medium) walirudishwa nyumbani kwa kukosa ada, chakula ndani ya nyumba kiliisha hadi chumvi kukosekana, gari lilikosa mafuta kwa kipindi kirefu n.k. Ila yeye alijikita kumtafuta Mungu katika Neno lake, na kumngoja kwa majira Yake. Katika kipindi hiki waliwahi kuishi kwa kula mahindi ya kuchemsha kwa muda usiopungua miezi mitatu.

Siku moja Mungu aliamua kumshangaza; mmoja wa waumini wake alifika nyumbani kuwatembelea na kuwafanyia manunuzi makubwa ya mahitaji ya chakula na kujaza gari lao mafuta. Huu ulikuwa muujiza kwa kuwa licha ya dhiki alizokuwa akipitia yeye na familia, hakuwahi kuwaambia watu juu hali halisi. Hapo ndipo alipozidi kujifunza kumtegemea Mungu katika maisha na huduma yake aliyoitiwa mpaka leo hii. Na huu ndio ulikuwa mwanzo wake wa kuinuliwa na kustawishwa kila sekta ya maisha. (Mathayo 6:33). Mtume Ndegi amekuwa na tafsiri yake rahisi ya Imani kuwa ni Kukubaliana na kile asemacho Mungu kwa 100%.

Msingi wa Huduma yake ya Kitume umejikita katika kuifundisha Kweli yote ya Mungu ili kutengeneza kanisa lile alilolikusudia Bwana Yesu alipokuwa akienda msalabani. Amejitoa kuusimamisha Ufalme wa Mungu ndani na nje ya Tanzania. Amekuwa akisisitiza kuwa Mkristo anapaswa kupata Fundisho sahihi ili awe mtu sahihi kuleta mabadiliko sahihi. Ni kupitia Neno la Mungu tu, ndipo mtu anaweza kufurahia na kupata faida za Ufalme wa Mungu.

Pamoja na Mtume Ndegi kufungua makanisa ya Living Water Centre (LWC) mikoani na Dar es Salaam, amekuwa akifundisha pia katika makanisa na huduma nyingine kwa kuwafikia watu wengi zaidi Tanzania na nchi nyingine kama Afrika Kusini, Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo n.k. Yeye na mke wake wamekuwa wakiendesha makongamano na semina kwa wanandoa, wanataaluma, wanaume, wanawake, wajawazito, wazee, vijana, wanavyuo, wachungaji, wafanyabiashara na viongozi. Mungu alimwongoza kuanzisha kozi maalum iitwayo “ Life Transforming” ambayo imelenga kuleta badiliko la kweli la kimaisha kwa mkristo kupitia Fundisho la Neno la Mungu. Kwa pamoja wasomesha wanafunzi na kuwalipia ada wale wale wenye matatizo ya jinsi hiyo. Mtume Ndegi amekuwa akitoa ushauri kwa hekima ya Kimungu kwa viongozi wa kiserikali na taifa kwa ujumla.